Chama cha muungano wa Kikristo nchini Nigeria kimeonya kutokea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, kufuatia mashambulizi ya mara kwa mara katika makanisa nchini humo. Baada ya mkutano wa viongozi wa makanisa, mkuu wa muungano huo Ayo Oritsejafor amesema kwa sasa wakristo wataanza kujilinda dhidi ya vita hivyo.
Onyo hili katika nchi inayojulikana sana kwa utajiri wake wa mafuta limekuja wakati ambapo kumekuwa na misururu ya mashambulizi ya mabomu na ufyatulianaji risasi unaofanywa na wanamgambo wa kundi la itikadi kali za kiislamu la Boko Harram. Mashambulizi hayo yalioanza siku ya krismasi mwaka jana yamesababisha vifo vya watu zaidi ya themanini.
Kundi la Boko Harram limetishia kufanya mashambulizi zaidi dhidi ya wakristo iwapo hawataondoka eneo la kaskazini mwa nchi hiyo,wanalodai ni jimbo la kiislamu. Kundi hilo linataka kuanzishwa kwa sheria mpya ya kiislamu kote nchini Nigeria.