Korea Kaskazini yatakiwa kumlinda Kim Jong Un hadi kifo

 

Korea Kaskazini imewaamuru raia wake na wanajeshi kumlinda kiongozi wao mpya, Kim Jong Un, hadi kifo ili kuimarisha ulinzi na kuendeleza sera ya siri ya kulitanguliza jeshi katika nafasi ya kwanza. Magazeti muhimu ya Korea Kaskazini yameandika katika makala maalum ya mwaka mpya kwamba chama, jeshi na umma unatakiwa kumlinda kiongozi huyo mpya mwenye umri karibu miaka 30 hadi kifo. Katika makala hiyo,magazeti  hayo yanasema mwaka mpya 2012 utaleta enzi ya neema  kwa Korea Kaskazini. Maafisa wa Korea Kaskazini pia wametaka wanajeshi wa Marekani waondoke Korea Kusini wakisema kuwepo kwao ni kikwazo kikubwa cha amani katika eneo la Korea.

Wakati huo huo Korea Kaskazini imekiri kuwapo matatizo  makubwa ya chakula yanayowakabili wananchi wake. Utawala wa nchi hiyo pia umesisitiza kuwa unataka kuendelea kuimarisha sera za kiongozi aliyeaga dunia wiki mbili zilizopita, Kim Jong Il. Hakuna matumaini ya kufanyika mageuzi katika taifa hilo lililotengwa na jumuiya ya kimataifa.

By Yericko Nyerere

Leave a comment